Sehemu ya 1.
Imeandikwa na M.M.Mwanakijiji
Nimekuwa mtetezi wa Muungano kiasi kwamba nimegundua nimebakia peke yangu. Wengine wanautetea Muungano kwa kutumia vitisho na wengine wanautetea kwa kutumia dharau. Binafsi ninaamini muungano unaweza kutetewa kwa hoja maridhiwa zenye kuonesha kuwa Zanzibar na wananchi wa Zanzibar wananufaika na wataendelea kunufaika zaidi katika Muungano kuliko nje ya Muungano. Kwamba hoja za kupinga muungano kwa madai kuwa Wazanzibari wanaonewa na kuwa Zanzibar inakaliwa kama koloni na Tanganyika haina mshiko, ni ya kupuuza na ina uwezo wa kuteka akili za watu wasiotaka kufikiria.
Baada ya muda mrefu kuwa mtetezi pekee wa Muungano kelele za hivi karibuni zimenibadili kabisa mawazo yangu na sasa nimekuwa na nitaendelea kushakizia muungano uvunjwe ili wale wanaoitaka Zanzibar yao wapewe na ili watu wa bara tuhangaike mambo mengine kuliko kuonekana tunawakandamiza Wazanzibari. Ile hofu ya Mwalimu kiasi cha kuachilia mambo mengi ya Zanzibar kuwa tukiungana kuwa nchi moja kamili kabisa Zanzibar watajiona wamemezwa imetimia kwani pamoja na kuwapa kila kitu Zanzibar bado wapo ambao wanaona wanamezwa!Ni kutokana na ukweli huu kwamba hakuna kiongozi au mwanasiasa wa Tanzania awe mzee au kijana mwenye uwezo wa kuutetea Muungano kisomi na kisiasa na kuwapinga wenye hoja dhaifu ndio maana leo naendelea na hoja yangu ya kuwasaidia Wazanzibar watoke kwenye Muungano, wawe na nchi na taifa lao na zaidi ya yote waweze baada ya kutoka kwenye Muungano kuanza mahusiano mapya na bara kama nchi mbili zilizo sawa. Ninaamini tunaweza kuhusiana vizuri zaidi baada ya Zanzibar kutoka na kuwa taifa lao wenyewe kuliko ilivyo hivi sasa ambapo Muungano hauteteleki – zaidi ya kutumia vitisho vya dola.
Tunawapenda sana ndugu zetu Wazanzibari kiasi kwamba hatutaki kuwang’ang’ania. Wapo kwao wenye kutuchukia sana kiasi kwamba hawataki hata kufikiria sisi ni ndugu zao. Wanatuangalia kwa dharau na kebeki wao wakiamini utukufu wao wa “Zanzibar” isiyokuwepo ndiyo tunu waliyonayo. Ukiwaskiliza sana baadhi ya wapinga muungano kwa kweli kabisa wamejawa chuki isiyo na kifani na chuki hiyo imezaa matunda meusi katika madhihirisho ya chuki dhidi ya watu wa Bara na Wakristu.
Lakini kitu kimoja ambacho watu wengi hawataki kukifikiria ni kuwa hawa watu wanaopinga Muungano wao wanadai “nchi”. Sasa hakuna aliyewauliza kwamba mbona katiba ya Zanzibar imefanyiwa mabadiliko na kuitangaza kuwa Zanzibar ni nchi? Sasa kama tayari Zanzibar ni nchi wanachodai hawa ni nini? Haiwezekani kuwa wanachodai ni nchi kwani nchi tayari wanayo na Katiba ya Zanzibar inasema hivyo! Wanachotaka siyo nchi! Wanachotaka ni kuwa nje ya Muungano! Hivi ni vitu viwili tofauti.Ndio maana basi katika makala ya leo nataka kuwasaidia Wazanzibari hawa na wale ambao wanaamini kuwa muungano haustahili kuteteewa kwa hoja bali kwa vioja. Pendekezo langu ni njia nyepesi za Wazanzibari kujiondoa kwenye Muungano bila kufanya maandamano, mihadhara wala kuwashtumu watu wa Tanganyika. Wazanzibari wakitaka kutoka kweli kwenye Muungano wanaweza kufanya hivyo ndani ya wiki chache tu na wakawa nchi. Nina uhakika serikali ya Muungano haitotumia nguvu kuwalazimisha kubakia! Nyerere mwenyewe alishasema kuwa hawezi kuwalazimisha Wazanzibari kubakia kwenye Muungano.
Njia ya kwanza Njia ya kwanza na nyepesi zaidi ya kuweza kujitoa kwenye Muungano ni kwa wananchi wa Zanzibar wakiongozwa na hawa wana- uamsho wawatake watendaji wote wa Muungano wenye asili ya Zanzibar kuachia nafasi zao mara moja na kurudi Zanzibar!
Hii ni pamoja na majaji, wabunge, mawaziri, maafisa wa polisi na vyombo vingine vya usalama, na wantedaji wengine ambao wako kwenye Muungano. Badala ya kuililia Tanganyika kila kukicha kuwa inawabana mashehe wa Zanzibari wenye kuongoza vuguvugu la kutoka kwenye Muungano waanzishe mihadhara ya kuwataka Wazanzibari wenzao ambao wanatumikia Muungano waachilie nafasi hizo.
Binafsi ningependekeza kama wataniruhusu waanzishe harakati hizo ili viongozi wote hawa waachilie nafasi zo ifikapo Disemba 10, 2012. Hii ni pamoja na Makamu wa Rais Ghaib Bilal, jaji mkuu na wengine.
Hawa wote wakishawishiwa kuondoka Wazanzibari wajiandae ama kuwapatia pensheni au kuwatafutia nafasi kwenye serikali ya nchi ya Zanzibar.
Sasa hawa wote wakikubali kuondoka kwenye nafasi zao za Muungano Zanzibar itapata wataalamu wengine wengi ambao wamekuwa wakitumikia Muungano na hivyo kujiongezea hazina ya wataalamu mbalimbali. Lakini pia itafungua ajira za Watanganyika wengi ambao wangeweza kushika nafasi zinazoshikiliwa na Wazanzibari hasa kwa vile Wazanzibari hao wako kimya na hawajitokezi kuutetea Muungano ambao wanautumikia.Pamoja na kuwataka viongozi wao na watendaji mbalimbali watoke kwenye Muungano katika harakati za mwanzo za Zanzibar kujitenga wana uamsho hawastahili kulalamikia Watanganyika. Hawahitaji kuendelea kuwaghilibu vijana wa Kizanzibari kuwa inanyonywa na sasa wanahitaji kupumua. Mashehe wa uamsho waende mbali zaidi katik akudai nchi yao. Waanze kuwahamasisha Wazanzibari walioko bara kuamua kuondoka bara na kurudi Zanzibar ili kuendesha shughuli zao huko.
Watu kama kina Bakheresa wenye biashara kubwa bara itabidi watiwe hamasa waamue kuondoka bara. Siyo hawa tu bali pia wale Wapemba na Wazanzibari waliona maeneo ya ardhi Bara. Hivi ndivyo ilivyotokea Sudan ya Kusini ambapo baada ya nchi hiyo kujitenga Wasudan ya Kusini waliokuwa wanafanya kazi Khartoum waliacha kazi zao na wengi wao wameamua kurudi kwenye nchi yao kuanza kuijenga.
Wengi tunakumbuka kuwa baada ya Rwanda chini ya Kagame kutulia kwa kiasi Wanyarwanda wengi ambao wengine waliishi kama Watanzania waliacha kazi zao na kurudi kwao Rwanda kuijenga nchi y ao. Nakumbuka baadhi ya wahadhiri kwenye taasisi mbalimbali nchini ambao tuliwadhania ni Wahaya au Waangaza walipoamua kuacha kazi zao kumbe walikuwa ni Wanyarwanda.
Hili pia litakuwa na faida kubwa sana kwa Zanzibar kwani itapata watu wengi zaidi wenye uwezo na utajiri mkubwa na vile vile itabidi iwaandalie viwanja vipya vya kilimo na makazi maana vile vya bara itabidi waviachilie kuwapisha Watanganyika ambao wanalalamikia kukosa ardhi au kupatiwa ardhi isiy nzuri. Na pia wafanyabiashara hao wa Kizanzibari watakaporudi Zanzibar na kama watataka kuja kufanya biashara Tanganyika itabidi waje kama wawekezaji na hivyo watasaidia katika ukuaji wa uchumi wa Tanganyika kama wageni wengine. Na kama watakuwa wajanja kama wageni wengine wanaweza kutengeneza mamilioni zaidi kuliko wanavyofanya sasa kama raia wa Tanzania!
Hivyo hilo ni jjambo la kwanza nawashauri wana uamsho; hamasisheni Wazanzibari waondoke Tanzania bara ili warudi Zanzibar ambako watapatiwa nafasi bora zaidi za ajira. Mtakapofanya hivyo, na watu wa Bara nao itabidi waanze kuondoka Zanzibar japo hapo nina uhakika kutakuwa na kazi kidogo. Watu wa Bara ni kina nani Zanzibar?
HUU NI MWANZO WA "LET ZANZIBAR GO MOVEMENT 2012"; Kama unaunga mkono kuwaacha Wazanzibar wajitoe kwenye Muungano weka kwenye sahihi yako "I support Let Zanzibar Go Movement 2012"! Tuwasaidie waharikishe wajitoe kwani hakuna kiongozi yeyote ambaye amekuwa na uwezo wa kuutetea Muungano kwa hoja maridhawa badala ya kutumia vitisho na mikwara.
No comments:
Post a Comment