Tuesday, June 26, 2012

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad:Hakuna Mzanzibari Atakayeadhibiwa Kwa Kutoa Maoni Yake Kuhusu Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Makamu wa Kwanza Wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akipokelewa na wafuasi wa Chama hicho alipotembelea ofisi za Chama hicho zilizopo Kilimahewa Jimbo la Kwamtipura
Makamu wa Kwanza Wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad akisisitiza jambo wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi waliojitokeza kumpokea alipofanya ziara ya kichama katika Jimbo la Chumbuni.Picha, Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza Wa Rais Zanzibar
---
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewahakikishia Wazanzibari kuwa hakuna mwananchi atakayeadhibiwa kwa kutoa maoni yake kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwapo atatoa maoni hayo kwa kufuata utaratibu uliowekwa.

Amesema Tume iliyoundwa kwa ajili hiyo, itakuwa ikipokea maoni yote yatakayotolewa na wananchi, na kutoa wito kwa wananchi kutogomea utoaji wa maoni, na badala yake wajitokeze kwa wingi kuwasilisha maoni yao kwa kadri wanavyotaka mabadiliko hayo yafanywe.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF ametoa wito huo kwa nyakati tofauti alipokuwa akitembelea majimbo ya uchaguzi ya Chumbuni na Kwamtipura katika Wilaya ya Mjini Unguja kuangalia uhai wa Chama hicho, ikiwa ni mfululizo wa ziara zake za kutembelea majimbo mbali mbali Unguja na Pemba.

Amesema njia pekee ya kuondoa kero za Muungano ni kwa wananchi kujitokeza kutoa maoni yao mbele ya Tume ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya katiba, na kwamba maoni yao yatazingatiwa, kuheshimiwa na kufanyiwa kazi kwa kadri watakavyoyatoa.

Amefahamisha kuwa wananchi watakuwa huru kutoa maoni yao, na kuwataka kuepuka jazba na kuvumiliana wakati wanapowasilisha maoni hayo, ili kuepusha malumbano yasiyokuwa ya lazima na ambayo hayatoisaidia nchi kwa njia yoyote, bali kuitia doa ambalo linaweza kuchukua muda mrefu kufutika.

Maalim Seif amewatahadharisha wananchi kuepuka vitendo vya vurugu na kuienzi amani iliyopo ambayo ni moja kati ya mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa serikali yenye mfumo wa umoja wa kitaifa.

Katika hatua nyengine, Katibu Mkuu huyo wa CUF amewakumbusha wazanzibari ambao bado hawajapata vitambusho vya ukaazi kuvifuatilia kwa nguvu zote kwa vile ni haki yao na ni muhimu katika maisha yao ya kila siku. “Naomba mufahamu kuwa vitambulisho hivi si kwa ajili ya kura tu, bali ni lazima muwe navyo wakati munapoomba ajira, kujiunga na elimu ya juu, kupata paspoti na hata kumiliki mali” , alitanabahisha Maalim Seif.

Ameonya kuwa watendaji wakorofi wanaokwamisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo bila ya sababu za msingi watachukuliwa hatua za kisheria, kwani watakuwa wamekiuka agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na sheria na taratibu za nchi. “Rais wa Zanzibar alisema kuwa kila Mzanzibari kwenye sifa za kupata kitambulisho lazima apatiwe kitambulisho hicho”, alikumbusha na kuhoji iwapo kuna mtu mwengine anayeweza kufanya vyenginevyo.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Chama hicho, Maalim Seif amesema chama kimepata maendeleo mazuri kutokana na uhai wa wanachama wake, na kuwataka viongozi wa majimbo na matawi kuendeleza utamaduni wa kufanya vikao ili kutatua changamoto zinazojitokeza ndani ya Chama pamoja na kutathmini maendeleo yao. Katika ziara hiyo, Maalim Seif pia alitembelea majimbo ya Kikwajuni, Rahaleo na Kwahani katika Wilaya ya Mjini.

Na
Hassan Hamad
Ofisi Ya Makamu wa Kwanza Wa Rais Zanzibar

No comments: