Friday, June 8, 2012

Mazishi Ya Mwenyekiti Mstaafu CUF Marehemu Musobi Mageni

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akitoa salaam za pole kwa viongozi na chama cha Wananchi CUF na wananchi wa mkoa wa Mwanza katika mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu Musobi Mageni
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akiweka udongo kwenye kaburi la Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu Musobi Mageni ,kulia kwake ni Mwenyekiti wa Cuf Profesa ibrahim Lipumba ambao wote walijumuika na viongozi na chama cha Wananchi CUF na wananchi wa mkoa wa Mwanza katika mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu Musobi Mageni
--
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amejumuika na viongozi wa chama cha Wananchi CUF na wananchi wa mkoa wa Mwanza katika mazishi ya Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, marehemu Musobi Mageni huko kijijini kwao Ngudu, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Katika mazishi hayo, pia alihudhuria Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, Makamu Mwenyekiti, Machano Khamis Ali, pamoja na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa, wakiwemo Waziri wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Haki za Binaadamu, Salum Bimani.

Marehemu Musobi alifariki Dunia Mei 30, mwaka huu nyumbani kwake Ngudu baada ya kusumbuliwa na maradhi ya shinikizo na damu na sukari kwa muda mrefu.

Marehemu alihamia chama cha Wananchi CUF mwaka 1994 na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Taifa mwaka 1995 hadi 1999 alipostaafu na kubaki kuwa Mjumbe wa kudumu wa Baraza Kuu la Taifa na Mkutano Mkuu wa chama hicho hadi kifo chake.

Katika uhai wake, marehemu aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini kuanzia mwaka 1972 hadi 1975, mwaka 1976 hadi 1978 Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala Rajan Industries Ltd. Nafasi nyengine ni alizowahi kushikilia ni Ubunge na Mkuu wa Wilaya katika wilaya ya Chunya, Kahama na Muleba.

Akitoa salamu za rambirambi, Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wakati wa mazishi alisema, marehemu alikuwa kisima cha busara na mwenye hekima kubwa na ndio maana viongozi wa CUF walikuwa wakikimbilia kwake kuchota ushauri wake.

“Huu ni msiba mkubwa sio tu kwa familia yake, bali kwa chama chetu na kwa serikali zote mbili”, alisema Maalim Seif.

Marehemu ambaye alizaliwa mwaka 1930, ameacha wajane wawili, watoto 15, wajukuu 28 na vitukuu sita.
Na
Khamis Haji
Ofisi Ya Makamu wa Kwanza Wa Rais Zanzibar

No comments: