Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete aliendesha harambee ya kuchangia taasisi ya Mkapa inayoitwa Mkapa HIV/AIDS Foundation, ambapo Mheshimiwa Rais, alifanikiwa kuchangisha kiasi cha shilingi bilioni 3.2 katika hafla hiyo, ambayo ilifanyika Jana, jumanne Juni 05,2012 usiku katika hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency iliyopo jijini Dar es salaam.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mzee Benjamin William Mkapa, ilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, Mashirika na Taasisi za Umma na Binafsi, ambapo kwa pamoja waliweza kuchangia kiasi hicho cha pesa. Lakini pia, hafla hiyo ilihudhuriwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Hata hivyo, Makusanyo hayo ya kiasi hicho cha bilioni 3.2 yalizidi kiwango cha makusudio ya awali ya harambee kwa asilimia sita (6%), ambapo malengo yalikuwa ni kuchangisha kiasi cha shilingi bilioni 3. Kiasi hicho cha pesa kitawezesha taasisi hiyo iliyojikita katika kusaidia jamii ya waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kuhamasisha na kufundisha njia mbalimbali za kujikinga na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment