CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimegeuza mashambulizi yake na safari hii kimekishutumu Chama cha Wananchi (CUF) kwa kile walichosema kuwahadaa Watanzania kiasi cha kuaminika kuwa ni wapinzani wa kweli.
Mashambulizi hayo yaliongozwa na viongozi wawili wa juu wa CHADEMA, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa wakati wa mikutano mikubwa waliyoifanya jana mkoani hapa.
Mbowe akifungua tawi la CHADEMA katika eneo la Mihuta wilayani Tandahimba alisema mwanzoni walidhani CUF kilikuwa na dhamira ya kweli ya kuwakomboa wananchi na ndiyo maana waliwaachia mikoa ya kusini kwa ajili ya kuendeleza kazi hiyo.
Aliongeza kuwa dalili za wazi za CUF kushindwa kuwatumikia watu wa kusini zimeonekana wazi baada ya kuamua kufunga ndoa ya mkeka baina yake na CCM.
“Ninachoweza kuwaambia wana Mihuta ni kwamba CHADEMA, CUF na CCM si baba yenu wala mama yenu na kama mtaona vyama hivi haviwasemei achaneni navyo, na kwa kuwa CUF na CCM mlivipa dhamana hiyo vikashindwa mviache sasa,” alisema.
Mbowe, amewataka wananchi wa wilaya ya Tandahimba kuihukumu serikali ya CCM kwa vile haitetei maslahi ya Watanzania hususan wakazi wa Tandahimba na sasa inatumia mabavu kuwatisha hata katika haki zao za msingi hususan pale wanapodai kulipwa kulingana na nguvu zao zilizotumika.
“Jamani Tanzania inasifika kwa kutajwa kuwa nchi inayofuata haki na sheria za binadamu lakini leo Wanatandahimba mnapigwa mabomu na askari wanaotumia kodi zenu kwa ajili ya kudai fedha za korosho ambazo kwa makusudi serikali imeamua kuwakopa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani,” alisema Mbowe.
Alibainisha kuwa hakuna haja ya wakazi wa Tandahimba na Mtwara kwa ujumla kulazimishwa mazao yao kuuzwa kupitia stakabadhi ghalani wakati mikoa mingine haifanyiwi hivyo na wanauza mazao kwa matajiri wanaowataka na bei wanayoitaka.
Dk. Slaa atoboa siri ya CUF
Naye Dk. Slaa alitoboa siri ya namna CUF ilivyoamua kuwa sehemu ya utawala, baada ya kufichua barua mbili zikiomba fedha kwa ajili ya kuhudumia chama na safari za kifamilia za Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Alisema barua ya kwanza ya Katibu Mkuu wa CUF Maalimu Seif kwenda serikalini inaomba kuwezeshwa kufanyika kwa mkutano wao wa chama kwa siku tatu katika eneo la Bagamoyo kwa gharama za sh milioni 34.
Dk. Slaa alisema barua ya pili ni ile inayoomba dola za Kimarekani 10,000 kwa ajili ya nauli ya kwenda Nairobi Kenya kwa mke wa Maalim Seif kwa safari ya kifamilia, ikiwa ni sawa na dola 1,000 kwa siku.
Aidha Dk. Slaa alisema katika taarifa hiyo inaonyesha pia kuna fedha za dharura kwa ajili ya matumizi ya Makamu wa Rais ambayo ni dola 3000 na kudai kuwa huo ni ufisadi usioweza kuvumiliwa na wapenda haki.
Alisema kwa mfumo huo wa CUF kutegemea hata katika mikutano yake ya chama fedha za serikali, ni ushahidi wa waziwazi kuwa inafanya kila kitu kwa kuongozwa na serikali ya CCM.
1 comment:
ikiwa hivyo ndivyo basi kazi
Post a Comment