Na Elias Msuya ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha, amesema vijana wengi nchini hawataki CCM kwa sababu hawaoni kilichofanyika tangu kilipoanzishwa.
Masha alisema wananchi wanahitaji kuona mabadiliko na kwamba, hali hiyo inatokana na kutosoma vizuri historia ya Tanzania. Akizungumza kwenye kipindi cha Mkasi kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha EATV, alisema hatua ya kutopenda chama hicho imetokana na vijana kutosoma historia.
“Vijana wengi hawaipendi CCM, wengi wanataka mabadiliko… siyo kosa lao, hawakufundishwa. Kuna wakati nilikuwa Chuo Kikuu cha St Augustine Mwanza nazungumza, kijana mmoja akasimama akasema nyie, wazee ndiyo wanarudisha nyuma nchi. Nikaangalia nyuma nikajiuliza huyo mzee yuko wapi... Nikagundua kumbe na mimi ambaye nilikuwa najiona kijana kniko kwenye kundi la wazee” alisema Masha.
Masha ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Fortunatus Masha, alisema vijana wengi wanapenda mabadiliko ya haraka jambo ambalo hawalioni ndani ya CCM na kuongeza kuwa, hali hiyo inasababishwa na kutokuwapo kwa mkakati wa kuwafundisha historia ya mafanikio ya Serikali na viongozi wake. “Leo hii ukienda Nairobi ukitaka kitabu kuhusu maisha ya Raila Odinga utaipata, ukitaka historia ya (Daniel) Moi .. Kenyatta utaipata. Mimi kijana wangu ana miaka 17 anasoma South Africa (Afrika Kusini) alikuja hapa anaomba kitabu ili nijue Tanzania imetoka wapi,..Hakuna,” alisema Masha na kuongeza:
“Sasa kama mtoto ambaye anataka kujua nchi yake, anakosa hata pa kuipata, nchi yake ikoje, marais waliotawala, tumefikaje hapa? Lazima waseme tumekuwa maskini kwa sababu ya chama ambacho kiko madarakani.”
Kuhusu kushindwa kwake ubunge mwaka 2010, Masha alisema amekubali kushindwa na anaendelea na kazi zake nyingine. “Ukiingia kwenye uchaguzi ni sawa tu na kuingia kwenye mpira, kuna kushinda na kushindwa, kikubwa ukishashindwa kubali matokeo endelea na maisha. Tatizo watu wengi na hasa wanasiasa wenzangu hawana kazi nyingine za kufanya,” alisema Masha.
Alipinga madai kuwa kipindi chake cha ubunge na uwaziri hakufanya lolote katika jimbo lake, badala yake alitoa mifano ya kazi alizofanya na kwamba, wanaoeneza hayo ni watu wenye fitina. “Sidhani kama ni kweli, unajua kwenye siasa kuna fitina imani yangu ni kwamba kazi yangu nilifanya na kazi yangu ya uwaziri niliifanya. Of course (bila shaka) kutokana na mfumo tulionao, mwenzako lazima akumalize ili akushinde,” alisema Masha na kuongeza:
“Leo hii tunapoongelea Nyamagana kuna chuo cha polisi kimejengwa, kuna Sekondari ya Mkolani imejengwa nje ya bajeti ya Serikali… ni kutoka kwa wafadhili na marafiki, there’s a lot of works (kuna kazi nyingi).” Alisema alikuwa akisomesha watoto 236 kwa mshahara wake wa ubunge na kwamba, tangu alipoingia bungeni mshahara wake ulikuwa ukipelekwa jimboni kusaidia wasiokuwa na uwezo.
“Leo hii ndiyo watu wanakumbuka, ndiyo nasema leo hii hata mke wangu na watoto wangu nao wafurahi kidogo kile ninachokipata, nipeleke kwenye maendeleo ya familia,” alisema. Hata hivyo, Masha alisema kazi za siasa zinahitaji uvumilivu hivyo alijitahidi kuvumilia changamoto hizo kipindi chote cha uongozi wake.
No comments:
Post a Comment