Friday, June 1, 2012

Samaki wanaovuliwa baharini wapungua

KUHARIBIWA kwa mazingira ya bahari kutokana na uvuvi usio endelevu na uchafuzi wa mazingira kumeelezwa kusababisha kushuka kwa kiwango cha samaki wanaovuliwa baharini kutoka tani 52,935 mwaka 2001 hadi tani 43,459 mwaka 2007.

Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dk. Terezya Huvisa wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika Juni 5 kila mwaka.
Alisema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa hivyo kusababisha sekta mbalimbali kuguswa na hali hiyo na kwamba makadirio ya haraka yanaonyesha kwamba nchi inahitaji takriban dola milioni 150 hadi 500 kila mwaka kukabiliana na tatizo hilo.

“Uchafuzi mjini pia ni tatizo kubwa hasa kwa miji yetu. Inakadiriwa kuwa tani 10,000 za taka ngumu huzalishwa kwa siku nchini kote na takriban asilimia 80 ya taka hizi hazitolewi na kutupwa zinakostahili hivyo napenda kutumia nafasi hii kutilia mkazo kampeni ya usafi.
Aliwataka wananchi wote kujitokeza kwenye shughuli za usafi siku ya Jumamosi asubuhi kuanzia saa moja hadi saa nne, na kueleza kwamba ni jukumu la kila halmashauri kusimamia zoezi la usafi ili kuiweka miji katika hali nzuri.
Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira kwa mwaka huu Dk. Huvisa alisema yatafanyika katika mkoa wa Kilimanjaro na kwamba lengo lake ni kuelimisha na kuhamasisha zaidi jamii kujikita kwenye uzalishaji endelevu

No comments: