Friday, June 1, 2012

Marufuku Kuvuta sigara uwanja wa Ndege JNIA!

MKURUGENZI wa kiwanja cha ndege cha Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Moses Malaki amepiga marufuku uvutaji wa sigara unaofanywa na watumiaji wa uwanja huo.
Moses aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa licha ya matangazo ambayo yamewekwa katika eneo hilo, bado kumekuwa na wimbi kubwa la wavutaji wa tumbaku ambao moshi wake umekuwa ukiwaathiri wavutaji na wale ambao sio wavutaji.
“Mwingiliano wa makampuni ya tumbaku umekuwa ukileta moshi mwingi kwenye kiwanja hiki cha ndege hali inayopelekea watu wasiovuta na wale wanaovuta kuathirika,” alisema Moses.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Ayubu Mgimba, ambaye ni mkurugenzi msaidizi wa wizara hiyo, alisema tumbaku imekuwa ni tatizo kubwa ambalo limekuwa likisababisha vifo vinavyozuilika.
“Ni ukweli usiopingika kuwa tumbaku ni sababisho kubwa la vifo vinavyozuilika hapa duniani ambapo takriban watu 800,000 hupoteza maisha kutokana na moshi wa tumbaku hivyo endapo serikali haitadhibiti hali hii hadi kufikiao mwaka 2030 vifo vitaongezeka hadi kufikia milioni 8 kwa mwaka,” alisema Mgimba

No comments: