Na Tausi Ally
WIKI iliyopita Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilitoa kibali cha ujenzi wa jumba la ghorofa 14 kwa mfanyabiashara Mustafa Jaffer Sabodo.
Kibali hicho kilikabidhiwa kwake na Meya wa Ilala, Jerry Silaa katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Lakini, unaweza kujiuliza, je, huyu Sabodo ni nani, ametokea wapi hadi kuweza kupata umaarufu ule alionao nao?
Swali hilo linajibiwa naye ambaye licha ya kupooza sehemu ya mwili wake mwaka 2000, ameendelea kufanya kile anachotaka ikiwemo kusimamia miradi yake na ya jamii kuhakikisha inafanikiwa.
Mei 14 mwaka huu, Sabodo alitimiza miaka 70, huku akiwa amekwishajitolea vitu vingi vya maendeleo kwenye jamii ya Watanzania ikiwemo kuwachimbia visima zaidi ya 280.
Anasema katika mahojiano kwamba hali hiyo aliyokuwa nayo haimzuii kufikia malengo yake.
Anasema yeye alizaliwa mwaka 1942 mkoani Lindi na kwamba ametoka kwenye familia yenye utajiri wa imani na fedha.
“Mimi nimetoka kwenye familia ya Uislamu wa Kihindi wa Gujarati Khoja, nilijitahidi kupambana dhidi ya umaskini nikiwa na matarajio ya kuwa tajiri na ninamshukuru Mungu nimekuwa hapa nilipo,”anasema.
Anafafanua kuwa licha ya kutoka kwenye familia ya utajiri baadaye alifilisika na akapambana dhidi ya kufilisika huko kwa kuweka matarajio ya kuwa tajiri kama alivyo sasa.
Akizungumza katika hafla ya kuzaliwa kwake, Sabodo anasisitiza kuwa hali yake aliyonayo kwa hivi sasa haimzuii kufanya chochote anachohitaji katika harakati za kuikomboa jamii inayohitaji msaada wa kuwekeza kwenye maendeleo ya muda na mfupi yakiwemo ya elimu na afya.
Kielimu, Sabodo anasema kuwa alisoma Shule ya Sekondari ya Lindi na baadaye alihitimu ngazi ya cheti kwenye Chuo cha Cambridge.
“Wakati nasoma nilikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi wazuri darasani katika kipindi hicho kwa kushika nafasi ya kwanza kati ya wenzangu wengi,”alijinasibu.
Akizungumza kwa tabasamu jepesi, wakati amepumzika nyumbani kwake, Upanga jijini Dar es Salaam, Sabodo ambaye jina lake lilianza kama utani kutokana na fujo zake anasema baadaye alihitimu Chuo cha Edinburg nchini Uingereza mwaka 1965 ambapo alisoma sheria ya biashara na usimamizi wa mifuko ya fedha.
‘Kozi hizi zilinisaidia mimi mwenyewe kujiletea mafanikio makubwa na kuwa mshauri wa kampuni, nimejikita zaidi katika masuala ya madeni ya kimataifa na uwezeshaji, “anasema.
Anaongeza kuwa yeye ni mmoja kati ya wafanyabiashara wakubwa na biashara zake zimesambaa kwenye nchi mbalimbali zikiwemo Tanzania, India, Ufaransa, Kenya, Sudan na Zimbabwe.
Anasisitiza kuwa kutokana na uchapakazi wake na kuamini katika ukweli amekuwa ni mtu mwenye mafanikio aliyoyatarajia kuyafikia na kwamba ameyafikia kwa kila kiwango ukitofautisha na matajiri wengine ambao utajiri wao umepatikana kwa bahati au kurithi kutoka kwa wazazi wao.
Anasema yeye hayupo kwenye kundi hilo ambalo wengi wao huutumia utajiri huo wa familia vibaya, kwa kuwa amezaliwa kwenye familia mashuhuri na kuondoa vikwazo vyote vinavyomfanya mtoto wa familia ya kitajiri kutafuta utajiri wake yeye mwenyewe.
Anafafanua kwamba mafanikio yake aliyapata kutokana na kujishughulisha. “Niliamua kupambana ili niwe hivi nilivyo sasa kutokana na kuvutiwa na mafanikio ya babu yangu, akiongeza kuwa alikuwa akitaka kuwa mtu tariji.
Baadaye niliishi nje ya Tanzania kwa kufanya kazi ya ushauri wa kimataifa na kurejea nchini mwaka 1996 na kuwekeza.
Anasema amezunguka nchi mbalimbali za Afrika, Asia , Ulaya na Mashariki ya Kati na kwamba sasa safari zake anazielekeza nchini India kwa ajili ya kupata matibabu.
Akizungumzia moyo wake wa kujitolea, Sabodo anasema mwaka 2003 alitoa udhamini wa uchezeshaji wa bahati nasibu ya mfuko wa Mwalimu J.K Nyerere wenye thamani ya Sh 100 milioni.
Anabainisha kuwa wazo la kuanzishwa kwa mfuko huo wa Mwalimu Nyerere lilikuwa ni lake, pia alichangia Sh 1.3 bilioni katika kuufanikisha.
Pia, anasema amechangia miradi mbalimbali ikiwemo kutoa kiasi cha Sh5 bilioni kwa ajili ya kuchangia chuo cha ualimu cha elimu ya juu cha Mtwara, alichangia Sh 965 milioni kwa ajili ya upanuzi wa majengo ya hospitali ya Shree Hindu Mandal, mradi wa Khoja Shia-aheri Sh 1.6 bilioni.
Ni wapi alikojifunza moyo huo wa kujitolea, naye anajibu, “Hakuna shule inayomfundisha mtu kutoa kitu, bali ni kitu kinachotoka moyoni mwake na unapokuwa unatoa unatengeneza nafasi ya wewe kupata.”
Kuhusu mafanikio yake, Sabodo anasema anamkumbuka babu yake ambaye alihitaji kuwa mkombozi wa watoto kwa kuwajengea kituo cha Ultra-Moderm katika kiwanja kilichopo karibu na makazi yake yaliyopo Mtaa wa Magore, Upanga.
Lakini, tumaini lake kubwa linategemea Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)ambalo limempatia mwekezaji mwingine eneo hilo.
Je, ameshauacha mradi huo, anajibu kuwa mradi huo ni wa faida ya watoto wanaohangaika kupata maeneo ya kupumzika na burudani hapa jijini Dar es Salaam.
“Sitaki kukata tamaa nitafuata taratibu zote kuhakikisha mradi huo unakamilika,” anaeleza.
Akizungumzia kuhusu misaada anayoitoa ikiwamo kwa vyama vya siasa kama CCM na Chadema, anasema misaada yake haina dini maalum bali inatolewa kwa ajili ya mioyo ya watu wanaohitaji na ya kibinaadamu.
Anasema dini yake yeye ni kupenda watu hususan wale wanaohitaji msaada kwa kuwawekea uwekezaji wa muda mrefu kama shule, hospitali pamoja na miradi ambayo itawanufaisha watu sawa ukiachana na dini zao.
Anawahamasisha watu wawe na moyo wa kujitolea kama wake, pia anasema aina yoyote ya utoaji ni muhimu kwa wanaohitaji kama vile pesa, muda, ujuzi, upeo na hata usikilizaji.
Kwa upande wa mchango katika elimu, anasema anajihusisha katika shughuli za uchumi na maendeleo ya kijamii kwa kutoa mabilioni ya Shilingi kwa kupunguza umaskini na kukuza miradi ya kijamii na afya.
Sabodo pia amejenga kituo cha elimu cha Sabodo Education Centre kilichopo kijiji cha Mayanda umbali wa kilometa 16 kutoka Mtwara mjini.
Sabodo ambaye anajenga jengo la ghorofa 14 la maegesho ya magari yenye uwezo wa kuegesha magari yapatayo 300 kwa wakati mmoja litakalogharimu dola za Kimarekani 3 milioni jijini Dar es Salaam, katika harakati za kupunguza tatizo la maegesho ya magari linalolikabili jiji la Dar es Salaam na kuboresha huduma hiyo.
Aprili 5, mwaka huu, Sabodo licha ya kuwa mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ametoa Sh 100 milioni kwa ajili ya kukipongeza chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),kwa ajili ya ushindi wa kiti cha ubungo alichoshinda Joshua Nasari wa jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha.
Pia alitoa baskeli 100 na kuahidi kuchimba visima vitano katika jimbo hilo
No comments:
Post a Comment